JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MSULUHISHI WA MIGOGORO YA BIMA

TIRA Logo
Msuluhishi wa Migogoro ya Bima ashiri­ki Mkutano wa Madalali wa Bima Zanzibar
26 Sep, 2025
Msuluhishi wa Migogoro ya Bima ashiri­ki Mkutano wa Madalali wa Bima Zanzibar

Msuluhishi wa Migogoro ya Bima Tanzania, Bi. Margaret Mngumi, ameshiriki kama Mgeni Maalumu katika Mkutano Mkuu wa Madalali wa Bima Tanzania uliofanyika jana, tarehe 25 Septemba 2025, katika hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar.

Katika salamu zake, Msuluhishi wa Migogoro ya Bima alibainisha kwamba ofisi yake ni chombo huru kilichoundwa kwa lengo la kusikiliza na kutatua malalamiko ya watumiaji wa huduma za bima kwa haki, haraka na kwa gharama nafuu. Alisisitiza kuwa majukumu ya Ofisi ya Msuluhishi ni muhimu katika kulinda maslahi ya wateja na kuongeza imani ya wananchi kwa huduma za bima.

Aidha, Bi. Mngumi alihimiza madalali wa bima nchini kuendelea kushirikiana na Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima pale panapojitokeza changamoto, akieleza kuwa migogoro si kikwazo bali ni fursa ya kujifunza na kuboresha huduma. Alisisitiza uadilifu, uwajibikaji na weledi kama nguzo kuu zitakazoinua sekta ya bima na kuimarisha uhusiano kati ya watoa huduma na wateja.

Mkutano huo uliowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya bima kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, ulitoa fursa kwa washiriki kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto na kuweka mikakati ya pamoja ya kukuza soko la bima nchini.

Bi. Mngumi alihitimisha kwa kuwataka wadau wote wa bima kuendelea kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima ili kuhakikisha sekta ya bima inakua, inapanuka na inatoa mchango chanya katika maendeleo ya taifa.