TIO watoa elimu ya usuluhishi migogoro ya bima Wiki ya Huduma za Fedha Tanga
Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima (TIO) tarehe 20 Januari 2026, imetoa elimu ya usuluhishi kwa wananchi katika Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yanayoendelea jijini Tanga. Elimu hiyo imelenga kuwajengea wananchi uelewa kuhusu namna ya kushughulikia na kutatua migogoro inayotokana na huduma za bima kwa njia ya haki, haraka na bila gharama kubwa.
Akizungumza katika maonesho hayo Msuluhishi Mwandamizi TIO Bw. Aloyce Mbunito alisema kuwa wananchi wamehamasishwa kufahamu majukumu ya Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima, hatua za kufuata wakati wa kuwasilisha malalamiko pamoja na umuhimu wa kuhifadhi nyaraka zote muhimu za bima. Pia wananchi wameelezwa haki na wajibu wao wanapotumia bidhaa za bima.
Maonesho hayo yamewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya fedha ambapo TIO imeendelea kutoa elimu kwa makundi tofauti ikiwemo wafanyabiashara, waajiriwa na wanafunzi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha huduma za fedha zinawafikia wananchi kwa uelewa mpana na ulinzi wa haki zao.
TIO SULUHISHO LA HAKI LA MIGOGORO YA BIMA
