JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MSULUHISHI WA MIGOGORO YA BIMA

TIRA Logo
TIO yaongeza wigo utoaji huduma; masjala ndogo zaanzishwa katika mikoa
27 Oct, 2025
TIO yaongeza wigo utoaji huduma; masjala ndogo zaanzishwa katika mikoa

Katika kuhakikisha huduma za Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima Tanzania (TIO) zinamfikia kila Mtanzania, ofisi hiyo imeanzisha Masjala ndogo ambazo zitapatikana katika Ofisi za Kanda za Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kwa ajili ya kurahisisha huduma mbalimbali, hayo yalibainishwa katika mafunzo ya Wasimamizi wa Masjala ndogo za TIO yaliyofanyika tarehe 26 Oktoba 2025 Kibaha, Pwani.

Awali, akifungua Mafunzo hayo Msuluhishi wa Migogoro ya Bima Tanzania Bi. Margaret Mngumi alisema hatua hiyo inalenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za usuluhishi wa migogoro ya bima katika maeneo mbalimbali nchini, bila wananchi kulazimika kufika makao makuu ambapo sasa wanaweza kusajili migogoro na kuhudumiwa kwa haraka na gharama nafuu.

Aidha, katika mafunzo hayo; mawasilisho kuhusu Ofisi, majukumu ya TIO na Sheria zinazotumika yaliwasilishwa lakini pia wasimamizi walielezwa wajibu wao katika kuhakikisha kila mtanzania anapata huduma za usuluhishi katika Masjala hizo ndogo kwa kushirikiana na maafisa kutoka Ofisi ya Makao Makuu - TIO. Mafunzo hayo pia yalikuwa na kipindi cha maswali na majibu kilichowezesha uelewa zaidi.

Masjala hizo ndogo zitapatikana katika Ofisi kumi (10) za kanda za TIRA zilizopo bara na visiwani Zanzibar; kwa habari mbalimbali kuhusu TIO tafadhali tembelea ukurasa wetu wa mtandao wa kijamii wa Instagram; tio_tz lakini pia tovuti yetu ambayo ni www.tio.tz.

#TIO Tunapokea, Tunachunguza na Kusuluhisha migogoro ya bima