JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MSULUHISHI WA MIGOGORO YA BIMA

TIRA Logo
Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima (TIO) tunashiriki Maonesho ya 12 ya Kimataifa ya Biashara Zanzibar
03 Jan, 2026
Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima (TIO) tunashiriki Maonesho ya 12 ya Kimataifa ya Biashara Zanzibar

Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima (TIO) imeshiriki kikamilifu katika Maonesho ya 12 ya Kimataifa ya Biashara yanayofanyika Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya shughuli za kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mapinduzi. Ushiriki huo unalenga kuelimisha wananchi, wafanyabiashara na wadau wa sekta ya bima kuhusu jukumu la TIO katika kusuluhisha migogoro ya bima kwa haki, uwazi na kwa gharama nafuu.

Kupitia maonesho hayo, TIO inatoa huduma mbashara kwa wananchi kwa kuwaelekeza namna ya kuwasilisha malalamiko yanayotokana na huduma za bima kati ya wateja na kampuni za bima. Maafisa wa TIO wamekuwa wakitoa elimu, kujibu maswali na kufafanua taratibu za usuluhishi, hatua inayosaidia kuongeza uelewa wa jamii kuhusu haki zao wanapotumia huduma za bima.

Aidha, TIO imeeleza kuwa lengo lake kuu ni kuhakikisha wateja wa bima wanapata haki kwa wakati bila kulazimika kufuata taratibu ndefu za kisheria. Huduma za usuluhishi zinazotolewa na ofisi hiyo zimekuwa chachu ya kuimarisha uaminifu kati ya wateja na watoa huduma za bima nchini.

Ushiriki wa Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima katika Maonesho ya 12 ya Kimataifa ya Biashara Zanzibar unaonesha dhamira ya Serikali katika kulinda maslahi ya watumiaji wa huduma za bima. Hatua hiyo pia inaongeza mwamko wa wananchi kushiriki kikamilifu katika sekta ya bima, sambamba na maadhimisho ya Siku ya Mapinduzi Zanzibar.