TIO mkoa kwa mkoa elimu ya usuluhishi wa Migogoro ya Bima
Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima (TIO), kwa kushirikiana na Kanda ya Ziwa Tanganyika – Katavi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), tarehe 21 Mei 2026 imetoa elimu kwa viongozi na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda kuhusu huduma za bima, majukumu ya TIRA na TIO, pamoja na taratibu za ushughulikiaji wa malalamiko na utatuzi wa migogoro ya bima.
Aidha, kikao hicho kimelenga kuongeza uelewa wa wadau kuhusu umuhimu wa bima katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisera, sambamba na kuimarisha ushirikiano katika kuwafikia wananchi kwa elimu sahihi ya bima na huduma za utatuzi wa migogoro. Halmashauri iliahidi kuendelea kushirikiana na TIRA na TIO katika utoaji wa elimu kwa wananchi ili kusaidia upatikanaji wa huduma bora na ulinzi wa haki za watumiaji wa huduma za bima.
Katika mwendelezo wa shughuli hiyo, TIO na TIRA pia wamekutana na viongozi wa waendesha boda boda na bajaji wa Mkoa wa Katavi na kuwapatia elimu kuhusu umuhimu wa bima, haki na wajibu wa wanufaika wa huduma za bima pamoja na mifumo ya utatuzi wa malalamiko na migogoro.
Aidha, wadau hao walisisitiza umuhimu wa TIO na TIRA kuendelea kutoa elimu kuhusu Bima ya Afya kwa Wote (UHI) ili kuongeza uelewa wa wananchi na kupunguza changamoto zinazotokana na taarifa zisizo sahihi kuhusu huduma za bima ya afya.
Msuluhishi wa Migogoro ya Bima, Bi. Margaret Mngumi ametoa shukrani kwa Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo Saqware kwa kuwezesha utekelezaji wa shughuli hizi, pamoja na Kanda ya Ziwa Tanganyika TIRA kwa uratibu na ushirikiano uliofanikisha utoaji wa elimu kwa wadau na wananchi.
TIO Suluhisho la haki la Migogoro ya Bima
