TIRA na TIO Watoa Elimu ya Bima kwa Wafanyakazi wa Hospitali ya Mkoa wa Tabora – Kitete
Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima (TIO), kwa kushirikiana na Kanda ya Magharibi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), leo tarehe 18 Mei 2026 imefanya kikao na uongozi wa Hospitali ya Mkoa wa Tabora – Kitete pamoja na kutoa elimu kwa wafanyakazi wa hospitali hiyo kuhusu uwepo wa TIRA na TIO pamoja na majukumu yao, ikiwemo utatuzi wa malalamiko na migogoro ya bima ya afya.
Jumla ya wafanyakazi 124 wamepata elimu hiyo inayolenga kuwajengea uelewa kuhusu nafasi yao kama wadau muhimu katika usimamizi wa haki ndani ya sekta ya bima. Elimu hiyo pia imelenga kuwawezesha kushiriki kutoa taarifa na elimu kwa wananchi, hususan wagonjwa na ndugu wanaofika hospitalini hapo.
Aidha, semina hiyo imelenga kupunguza changamoto ambazo TIO hukutana nazo wakati wa kushughulikia migogoro inayotokana na madai ya ajali za barabarani pamoja na bima ya afya. Washiriki walielezwa umuhimu wa nafasi yao katika kulinda haki za wananchi wanaopata ajali za barabarani na wale wanaotumia huduma za bima binafsi pamoja na UHI.
Miongoni mwa mambo ambayo yamesisitizwa ni umuhimu wa kuwasaidia wananchi kutunza nyaraka muhimu zinazothibitisha gharama za matibabu, pamoja na kuhakikisha taarifa za mwisho za kitabibu zinaonyesha kwa usahihi kiwango cha ulemavu uliotokana na ajali na namna unavyoweza kuathiri uwezo wa mhusika kutekeleza majukumu yake.
Washiriki wa semina hiyo wameombwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa TIRA na TIO, huku wakifahamishwa kuhusu uwepo wa simu ya bure ya TIO, Ofisi ya Kanda ya TIRA pamoja na tovuti za taasisi hizo zinazoweza kutumika kupata elimu na taarifa mbalimbali za bima.
Vilevile, wameelezwa kuwa kwa sasa wananchi wanaweza kutumia mfumo wa kielektroniki kusajili migogoro ya bima kwa urahisi zaidi.
TIO suluhishi la haki la Migogoro ya Bima
